Kanuni za Usawa katika Urejeshaji

Kanuni hizi zinatumia matakwa na majukumu yaliyoelezwa katika Mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu katika sekta isiyo rasmi ya taka.

Kanuni hizi zilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Shift (2022) Executive Summary: Principles for Corporate Engagement with the Informal Waste Sector – Applying the UN Guiding Principles on Business and Human Rights to the Plastic Packaging Recycling Value Chain. Endapo utanakili kanuni hizi, tafadhali taja ripoti hii kama chanzo.

Unaweza kupakua Kanuni hizi kwa Kiswahili, Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza na Kireno.
Kanuni za Ushirikiano wa Mashirika na Sekta Isiyo Rasmi ya Taka Zinazolingana na Mwongozo wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Biashara na Haki za Binadamu (UNGP)

 • Wakusanyaji taka hutekeleza jukumu muhimu katika uchakataji tena wa taka ulimwenguni – wakikusanya na kuainisha hadi asilimia 60 ya taka ya plastiki inayochakatwa tena. Hata hivyo, wafanyakazi hawa mara nyingi hupata madhara mabaya zaidi yanayohusiana na haki za binadamu na wao ni baadhi ya wafanyakazi walio hatarini zaidi katika minyororo yote ya thamani katika biashara ulimwenguni. Ili kutimiza kanuni hii katika hali halisi, wahusika wa serikali na wa kibinafsi wanahitaji kuwajumuisha wakusanyaji taka kama wadau muhimu na wanaostahiki – na maslahi na matatizo yao kama masuala ya msingi – katika majadiliano na nyanja za utungaji sera za ujirani, kitaifa na kimataifa na katika maamuzi ya kibiashara.

 • Kampuni zote zilizo katika minyororo ya thamani ya uchakataji tena wa vifurushi vya plastiki zinapaswa kuchukua hatua zinazofaa kuzuia, kupunguza na kurekebisha madhara yanayosababishwa au kuchangiwa na kampuni hizo, na kujitahidi kuzuia na kupunguza madhara ambayo huenda yanahusiana na shughuli, bidhaa au huduma za kampuni hizo, kulingana na wajibu wa kampuni hizo katika haki za binadamu.

  Kampuni katika safu na sekta zote za minyororo hii ya thamani sharti zitambue sekta isiyo rasmi ya taka kama sehemu ya mnyororo wa thamani wa kampuni hizo zenyewe. Ukweli huu unahusu kampuni zilizo katika ncha zote mbili za mnyororo wa thamani – zile zinazotengeneza au kutumia taka ya plastiki ambayo hatimaye huopolewa na wakusanyaji taka, na zile zinazotumia vitu vilivyochakatwa tena kutokana na taka iliyoopolewa na wakusanyaji taka. Madhara yanayohusiana na haki za binadamu yanayowapata wakusanyaji taka bila shaka yanahusiana na wajibu wa kampuni hizo kuheshimu haki za binadamu kulingana na Mwongozo wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Biashara na Haki za Binadamu (UNGP), wajibu unaotanda katika mnyororo mzima wa thamani wa kampuni hizo. Kiwango cha madhara yanayohusiana na haki za binadamu na uwezekano mkubwa wa wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka kudhuriwa unaashiria kwamba, kwa kampuni nyingi kama hizi, madhara yanayohusiana na haki za binadamu yanastahili kukabiliwa kama suala muhimu la haki za binadamu.

 • Wahusika kutoka sekta ya umma na ya kibinafsi katika hatua zote za minyororo ya thamani ya uchakataji tena wa vifurushi vya plastiki – kuanzia utengenezaji na matumizi, udhibiti wa taka hadi uchumi rejeshi – wanastahili kuchukulia kwamba, angalau, wanahusika na athari hizi kwa wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka. Kupatikana kwa matokeo ya maana zaidi kwa wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka kutahitaji ushirikiano baina ya wahusika hawa, ijapokuwa wanaweza kuhusika na athari kwa wakusanyaji taka kwa njia tofauti (kusababisha, kuchangia au kuhusiana) na wanaweza kuwa na wajibu tofauti wa kutekeleza katika kubuni, kutekeleza na kuunga mkono mbinu zinazofaa.

 • Sheria na sera za nchi na mamlaka za umma, katika ngazi za kitaifa na za chini, zina wajibu muhimu katika kuweka muktadha, miundomsingi, mazingira ya kazi na hali ya kijamii kwa wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka. Kupatikana kwa matokeo ya maana kwa wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka kutahitaji serikali zitimize wajibu wao uliopo wa haki za binadamu kuhusiana na wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka, ikiwa ni pamoja na kuhimiza: uwezo wao wa kupata huduma za umma na mifumo rasmi ya usalama wa kijamii; kulindwa kwao dhidi ya kubaguliwa na kutengwa katika jamii; na kujumuishwa kwao kama wadau na wahusika muhimu katika michakato ya kuelekeza mifumo ya sheria na sera zinazosimamia udhibiti wa taka. Kukosa kuchukua hatua hizi kunaweza kuwaathiri wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka moja kwa moja; kunaweza pia (na mara nyingi huwa ndivyo) kuleta matishio makubwa zaidi ya kimuktadha ya madhara yanayohusiana na haki za binadamu kwa wafanyakazi. Kampuni zinapaswa kutumia na kujenga uwezo wao, kama inavyofaa kulingana na jinsi zinavyohusika na madhara hayo, kushirikisha wahusika wa serikali kutimiza matarajio haya katika hali halisi.

 • Kushirikisha wadau wanaoathirika ni suala kuu katika dhana ya uangalifu unaostahili wa haki za binadamu. Kampuni zilizo katika minyororo ya thamani ya uchakataji tena wa vifurushi vya plastiki zinapaswa kuwashirikisha wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka kwa njia ya maana na inayowaheshimu, kwa njia zinazotambua hadhi yao kama wanadamu, ili kuchangia uelewa wa kampuni hizo kuhusu matishio na madhara na katika kupanga jitihada za kuzuia na kukabiliana na madhara hayo. Mbinu za kufanya hivyo huenda zikawa tofauti katika safu mbalimbali za mnyororo wa thamani. Kwa kampuni za udhibiti na ukusanyaji wa taka, huenda ikahitaji juhudi kubwa za kujenga ushirikiano wa moja kwa moja na wakusanyaji taka huku zikikabiliana na hali ya kutoaminiana iliyopo. Kwa kampuni zilizo katika hatua za awali au baadaye zaidi (kama vile wazalishaji na wauzaji wa utomvu, watengenezaji wa bidhaa za plastiki iliyochakatwa tena na watumiaji wa plastiki, zikiwemo kampuni za bidhaa zitumiwazo mara kwa mara), inaweza kumaanisha kuwashirikisha wawakilishi halali wa sekta isiyo rasmi ya taka au mawakala wa kuaminika wa maoni yao, ili kusawazisha matarajio na vitendo.

 • Wanawake wakusanyaji taka wanakabiliwa na hatari maalum. Madhara yanayohusiana na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na yale yanayoathiri usalama na ulinzi wa kibinafsi, ubaguzi na unyanyasaji, na madhara mengineyo kwa riziki zao, yanapaswa kuchunguzwa na kushughulikiwa kwa mtazamo wa kimakusudi wa kijinsia. Hili linahitaji kuwashirikisha wanawake wakusanyaji taka, au mawakala wa kuaminika wa maoni yao, ili kuelewa jinsi haki zao zinavyokiukwa na njia bora za kukabiliana na hali hii.

 • Tukizingatia uanuwai wa minyororo ya thamani ya uchakataji tena wa vifurushi vya plastiki, jinsi minyororo hiyo ya thamani inavyobainika katika maeneo mahususi na nafasi ya sekta isiyo rasmi ya taka katika minyororo hiyo ya thamani, mbinu faafu zitahitaji kuelekezwa na, na kuzingatia miktadha ya mashinani. Wakati huo huo, mbinu za mashinani zinapaswa kuongozwa na upatanifu wa kimataifa kuhusu kanuni, pamoja na kushirikishwa kwa upana zaidi kwa wahusika katika minyororo hiyo mizima ya thamani. Kutimiza kanuni hii katika hali halisi kutahitaji kufafanuliwa kwa minyororo ya thamani ya mashinani ili kuelewa wahusika katika minyororo hiyo ya thamani, athari wanazopata wakusanyaji taka na mfumo wa sheria na sera za eneo zinazobainisha mazingira ya wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka. Kunazo mbinu mbalimbali za ushawishi zinazoweza kutumika, ikiwa ni pamoja na kubainisha matarajio kwa watoa huduma na wauza bidhaa, kuwashirikisha wabia wa biashara, kukuza uwezo, kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Serikali, kuhimiza maoni ya wafanyakazi, kushirikiana na kampuni sawa, kuboresha uwazi wa minyororo ya ugavi, kuwekeza katika kujenga umadhubuti wa minyororo ya ugavi na kutetea kanuni za kufaa zinazohimiza taratibu za biashara zinazoheshimu haki za binadamu.

 • Mara nyingi, wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka wametengwa kabisa na michakato ya kufanya maamuzi yanayoathiri maisha yao. Kampuni haziwezi kuhakikisha kuwa wawakilishi na maoni ya wakusanyaji taka yamejumuishwa katika michakato ya utungaji sera inayoongozwa na serikali. Hata hivyo, biashara zinaweza na zinastahili kutumia ushawishi wazo zenyewe kutetea kujumuishwa kwa wawakilishi wa wakusanyaji taka katika majadiliano na nyanja za utungaji sera, katika ngazi za mashinani, kitaifa na kimataifa. Ambapo juhudi hizi hazifanikiwi, kampuni bado zinastahili kujitahidi kuhakikisha kuwa maslahi na matatizo ya wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka yanazingatiwa na yanaelekeza michakato ya kufanya maamuzi.

 • Kampuni zilizo katika safu mbalimbali za mnyororo wa thamani zinapaswa kutafuta njia za kuhimiza ujumuishwaji zaidi wa sekta isiyo rasmi ya taka katika minyororo rasmi zaidi ya thamani ya sekta ya kibinafsi, kulingana na muktadha wa eneo. Hata hivyo, urasmishaji haustahili kufanywa sharti kwa wakusanyaji taka ili waweze kuendelea kupata taka ya kuchakata tena. Kanuni hizi zinanuiwa kuhimiza biashara katika minyororo yote ya thamani ya uchakataji tena wa vifurushi vya plastiki zishirikishe na ziwekeze katika minyororo hii ya thamani ili kujenga uwezo, kuendeleza ufanisi zaidi na kukuza unyumbufu zaidi, kwa kuzingatia maoni ya wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka.

 • Madhara yanayohusiana na haki za binadamu kwa wakusanyaji taka ni ya kimfumo. Madhara hayo hayasababishwi na shirika moja au uamuzi mmoja wa kibiashara, ijapokuwa maamuzi kama hayo yanaweza kuongeza tishio la athari mbaya iwapo hayaelekezwi na uangalifu unaostahili. Kuna vyanzo mbalimbali ambavyo kwa pamoja huwaweka wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka hatarini na kuwaletea madhara yanayohusiana na haki za binadamu. Kampuni zilizo katika minyororo yote ya thamani ya uchakataji tena wa vifurushi vya plastiki zinapaswa kuchunguza desturi zao za biashara – kuanzia taratibu za ununuzi, mahusiano katika mnyororo wa ugavi, hadi shughuli za ushawishi wa sera na zaidi – na jinsi zinaweza kuwa zinachangia madhara mahususi. Kampuni hizi pia zinastahili kuchunguza jinsi hali pana ya masoko (ikiwa ni pamoja na jinsi bei zinavyowekwa na wafanyakazi kulipwa) inavyoweza kuweka vizuizi vilivyojikita vya kiuchumi kwa desturi zinazoheshimu haki za binadamu, na ziwe tayari kushirikiana na wengine kushughulikia hali hizi.

Kiambatisho A: Maelezo ya madhara ya kawaida yanayohusiana na haki za binadamu yanayowapata wakusanyaji taka

Wakusanyaji taka wamechangia pakubwa katika udhibiti na uchakataji tena wa taka kihistoria na sasa, na washiriki wengi katika sekta hii wana ujuzi na tajiriba pana. Hata hivyo, licha ya jukumu muhimu wanalotekeleza katika mazingira na afya ya umma, wakusanyaji taka mara nyingi hupata madhara makubwa yanayohusiana na haki za binadamu. Katika Mwongozo wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Biashara na Haki za Binadamu (UNGP), haki za binadamu ambazo zinatumbuliwa kimataifa zimefafanuliwa katika Sheria ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na kanuni za msingi za Shirika la Kazi Duniani (ILO)3. Orodha hii inatoa maelezo ya madhara ya kawaida (ila si yote) yanayowapata wakusanyaji taka katika mnyororo wa thamani wa plastiki, pamoja na hali zinazoongeza ukali au uwezekano wa madhara hayo kutokea katika hali halisi4. Ijapokuwa si madhara na hali hizi zote zitawahusu wakusanyaji taka katika miktadha yote, madhara haya kwa wakusanyaji taka yanayohusiana na haki za binadamu mara nyingi huwa mabaya sana.

 • Kila mtu ana haki ya kuwa na kiwango cha maisha kinachotosheleza afya na uzima wake na wa familia yake, ikiwa ni pamoja na chakula na lishe ya kutosha, mavazi, makazi na uwezo wa kupata huduma za matibabu inapohitajika. Kwa wakusanyaji taka, kuna hali kadhaa ambazo zinaweza kuathiri uwezo wao wa kufurahia haki hii.

  • Mapato Duni: Mbali sana na takwimu ya ‘mapato ya kutosha’5, wakusanyaji taka wengi huishi chini sana ya kiwango cha umaskini katika nchi zao. Wao hulipwa kwa ajili ya vitu wanavyotoa, lakini si kwa kazi yao au huduma wanayotoa kwa umma kwa kukusanya taka.
  • Kutokuwa na Uwezo wa Kujadiliana katika Uamuzi wa Bei: Bei za taka iliyochakatwa tena mara nyingi huamuliwa na wakusanyaji wakubwa wa taka wanaonunua taka iliyochakatwa tena kutoka kwa wakusanyaji taka6. Wakusanyaji taka mara nyingi hawana uwezo wa kujadiliana ili kuweka bei ya haki, kwa sababu mara nyingi wanawategemea wakusanyaji wakubwa kufikia soko (hasa ambapo wakusanyaji wakubwa ndio pekee wanaweza kusafirisha taka).
  • Mapato Yasiyotegemeka: Kutokuwa na uwezo wa kujadiliana bei, kutokuwepo kwa mikataba imara katika sekta isiyo rasmi, na mchango wa hali katika soko pana ambazo zinaathiri mahitaji ya bidhaa (kama vile bei ya mafuta yasiyosafishwa), husababisha wakusanyaji taka kutokuwa na mapato ya kutegemeka au thabiti.
  • Kutokuwa na Uhakika wa Mapato: Pamoja na masuala haya, wakusanyaji taka huwa na wasiwasi kuhusu, na wakati mwingine huripoti kuwa wamepitia, hali ya kukosa riziki kwa sababu ya kuondolewa kwenye soko katika hali za ubinafsishaji wa sekta ya taka, mipango ya Wajibu Mpana wa Watengenezaji (EPR) ambayo haijajumuisha sekta isiyo rasmi ya taka, na kutojumuishwa katika minyororo ya ugavi ya ununuzi wa serikali na sekta ya kibinafsi.

  Kutokuwa na mapato ya kutosha, ya kutegemeka na hakika – pamoja na kutengwa na huduma za kijamii na za kifedha zilizotajwa hapo chini – kuna athari ya ziada ya kuwawekea vizuizi wakusanyaji taka ili wasiweze kuongeza mapato yao kwa “kupanda” katika mnyororo wa thamani. Wakusanyaji taka mara nyingi hawawezi kupata rasilimali za kifedha, vifaa, mafunzo, usafirishaji na ardhi inayohitajika kuhifadhi na kukusanya taka ya kuchakatwa tena.

 • Si wakusanyaji taka wote wanalenga kurasmisha biashara zao kupitia vyama vya ushirika, miungano au vyama vya wafanyakazi. Hata hivyo, wanapofanya hivyo, wanaweza kukumbana na vizuizi katika kujiratibu kama biashara za pamoja, ikiwa ni pamoja na rasilimali za kifedha zinazohitajika kujiratibu. Uwezo wa kujiratibu mara nyingi unafahamika kuwa haki wezeshi ambayo ikishughulikiwa inaweza kusaidia kuzuia na kukabiliana na madhara mengine yanayohusiana na haki za binadamu.

 • Wakusanyaji taka wanafahamu unyanyapaa unaohusiana na kazi yao. Mara nyingi wao huchukuliwa kama “watu wa chini” katika jamii na mara nyingi hupuuzwa au kudhulumiwa na wengine – tabia za ubaguzi ambazo zinaonekana kukubaliwa katika jamii nyingi. Hali hii ya kupoteza hadhi ya msingi ya mwanadamu ndicho kiini cha madhara yanayohusiana na haki za binadamu, na ndiyo chanzo na zao la madhara yanayohusiana na riziki, afya na usalama na hali nyingine za kikazi. Unyanyapaa unaweza pia kuathiri uwezo wa wakusanyaji taka kupata taka ya kuchakatwa tena.

 • Msingi wa kulindwa kwa haki nyingi za binadamu ni wazo kwamba watu wanastahili kutoa shauri na kujumuishwa katika maamuzi yanayoathiri maisha yao. Wakusanyaji taka wametengwa katika jamii na mara nyingi hawatambuliwi kama wadau muhimu na wanaostahiki. Mara nyingi ushauri wao hautafutwi katika michakato ya utungaji wa sera zinazoelekeza sekta ya ukusanyaji taka, wala katika upangaji na utekelezaji wa mipango au hatua za kampuni za kukabiliana na madhara yanayoweza kuwapata.

 • Kwa sababu sekta hii si rasmi, wakusanyaji taka mara nyingi hawajumuishwi katika ulinzi wa kijamii, ikiwa ni pamoja na usalama wa kijamii na huduma za afya. Wafanyakazi katika sekta zisizo rasmi, ikiwa ni pamoja na wakusanyaji taka, mara nyingi hawawezi kupata huduma za mifumo rasmi ya benki, na hata vitambulisho wakati mwingine. Hali hii ya kutojumuishwa kifedha pia inakuwa kizuizi kingine cha mapato thabiti na ya uhakika, kwa sababu sehemu rasmi zaidi za uchumi mara nyingi hazina nyenzo za kushirikisha sekta isiyo rasmi.

 • Katika miktadha fulani, ajira ya watoto ni sehemu ya sekta isiyo rasmi ya taka. Ingawa si kazi zote zinazofanywa na watoto huwa ajira ya watoto, ambapo watoto wapo katika sekta hii, mara nyingi huwa wanafanya kazi yenye hatari na/au hawawezi kupata elimu kwa sababu ya kazi hiyo. Watoto wanaweza kuandamana na wazazi wao kazini kwa sababu inaonekana salama zaidi kuliko kuwaacha nyumbani au kwa sababu wazazi hawawezi kupata huduma nafuu za utunzaji wa watoto na kwa urahisi. Hata ambapo watoto hawafanyi kazi, bado wanaweza kuwa hatarini wanapoandamana na wazazi au walezi wao ambao ni warejeshaji na kupata madhara kwa usalama na/au elimu yao.

 • Mazingira mabaya ya afya na usalama kazini katika ukusanyaji taka mara nyingi husababisha majeraha na hata vifo vya wakusanyaji taka wakati mwingine. Kwenye majalala, wakusanyaji taka hufanya kazi katika mazingira hatari, hukaribiana na bidhaa zinazoweza kuwadhuru na mivuke ya sumu, hawana vifaa maalum vya kujikinga (PPE) na wapo katika hatari ya kujeruhiwa vibaya na magari na vifaa vizito. Katika miktadha mingine, usalama na ulinzi binafsi wa wakusanyaji taka – hasa wanawake – upo hatarini, hususan ukusanyaji unapofanyika usiku.

 • Wakusanyaji taka hufanya kazi kwa saa nyingi mno, mara nyingi wiki nzima bila mapumziko, katika mazingira yasiyo na vyumba vya kujisaidia na huduma za msingi za usafi wa mazingira, hali ambayo pia inaweza kuwaathiri wanawake zaidi.

1Katika ripoti hii, istilahi ‘sekta isiyo rasmi ya taka’ na ‘wakusanyaji taka’ zinarejelea kundi la wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi wanaokusanya, kuainisha na kuongeza thamani ya taka inayoweza kuchakatwa tena kutoka vyanzo vya taka vya baada ya matumizi. Kihistoria, majina mbalimbali yametumiwa kama visawe kwa kundi hili, ikiwa ni pamoja na yale yaliyotumika hapa na vilevile ‘wafanyakazi walio katika mifumo ya ushirika au isiyo rasmi’ (kwa mujibu wa agizo la makubaliano ya Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa kuhusu plastiki – angalia UN Doc UNEP EA.5/Res.14)

2Washirika wa mradi wanatambua kwamba kanuni hizi ni matokeo ya mchakato uanozingatia minyororo ya thamani ya uchakaataji tena wa vifurushi vya plastiki, lakini yamkini zinaweza pia kutumika kwa taka za aina nyingine ambazo zinaweza kuchakatwa tena.

3Mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu (UNGP) hutumika kwa ‘haki zote za binadamu zinazotambuliwa kimataifa’ kumaanisha zile zilizo katika Sheria ya Kimataifa ya Haki za Binadamu (yaani, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na Maagano Mawili ya Kimataifa yanayoweka kanuni zake), pamoja na kanuni zinazohusu haki za msingi zilizo katika makubaliano nane msingi ya ILO kama ilivyoelezwa katika Azimio la ILO la Haki na Kanuni za Msingi Kazini.

4Orodha hii inanuiwa kuwa kielelezo wala si orodha ya matukio mahususi ya madhara; tathmini zaidi inahitajika kubainisha hali katika minyororo ya thamani ya kampuni mahususi.

5Mapato ya kutosha yanalingana na ujira wa kutosha kwa wafanyakazi wa kujiajiri. Wakusanyaji taka wakati mwingine hujiratibu katika vikundi vya ushirika au miungano, lakini wao si waajiriwa rasmi.

6Kwa jumla hutegemea bei zilizopo sokoni na ubora wa kinachouzwa.

Onyesha Nia

Iwapo ungependa kuwa mshiriki wa Usawa katika Urejeshaji tungependa kusikia kutoka kwako.

Onyesha Nia