Juhudi za Biashara

Kampuni zinazoshiriki katika mpango huu zimeshikamana kuunga mkono Taarifa hii ya Uzinduzi na Kanuni za Usawa katika Urejeshaji, ili kudhihirisha kujitolea kwetu kwa suala hili na kuhimiza kwamba Kanuni za Usawa katika Urejeshajii zikubaliwe kwa upana zaidi na zitekelezwe kwa dharura.  

Unaweza kupakua Taarifa yetu ya Uzinduzi kwa Kiswahili, Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza na Kireno.
Taarifa ya Uzinduzi

Kama kundi la kampuni zinazoongoza za bidhaa zitumiwazo mara kwa mara (FMCG) – Kampuni ya Coca-Cola, Nestlé, PepsiCo na Unilever – tumejitolea kuheshimu haki za wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi ya taka. Hivi leo tunazindua Kanuni za Usawa katika Urejeshajii na tunatoa wito kwa wengine, ikiwa ni pamoja na kampuni za bidhaa zitumiwazo mara kwa mara, kampuni katika sekta nyingine na biashara zilizo katika mnyororo mzima wa thamani zijiunge nasi.

Katika nchi nyingi, wafanyakazi hawa hutekeleza jukumu kubwa na muhimu katika ukusanyaji, uanishaji na uchakataji tena wa taka ya vifurushi na wa aina nyingine. Licha ya hayo, wapo hatarini kupata madhara mbalimbali yanayohusiana na haki za binadamu; hii ina maana kwamba huku uchakataji wa taka ukileta matokeo mema katika mazingira, unahitaji tathmini na ufuatiliaji zaidi wa haki za binadamu kutoka kwa kampuni zinazohusika katika minyororo ya thamani ya taka ya plastiki au ya uchakataji taka. Hata hivyo, kufikia sasa, tasnia na serikali, kwa pamoja, hazijajishughulisha vya kutosha au kukabiliana vilivyo na athari za sekta hii kwa hali ya kijamii na haki za binadamu. Huku tukijitahidi kukomesha uchafuzi unaotokana na plastiki – ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kubuniwa kwa mkataba kabambe na faafu wa kimataifa – ni sharti pia tujitahidi kujenga uchumi rejeshi wa plastiki ulio na usawa zaidi.

Kama biashara, sote tumekuwa tukichukua hatua nchini na kimataifa kukabiliana na athari za kijamii za sekta isiyo rasmi ya taka. Hata hivyo, tunatambua haja ya mbinu za mshikamano na ushirikiano zaidi katika mnyororo mzima wa thamani ili kushughulikia athari hizi kwa mafanikio. Tumeshirikiana na Tearfund (shirika la kiraia linalotetea kutambuliwa na kuheshimiwa zaidi kwa haki za wakusanyaji taka) kuendeleza majadiliano na ushirikiano katika masuala haya na kujumuisha maoni ya wamiliki wa haki. Nyenzo za Muungano wa Kimataifa wa Wakusanyaji Taka na za shirika la Wanawake katika Ajira Isiyo Rasmi: Kutandawazisha na Kuratibu (WIEGO) zilichangia sana katika mchakato huu.

Kundi letu, kwa ushirikiano na Shift, limebuni Kanuni za Usawa katika Urejeshaji. Kanuni hizi zinatumia majukumu yaliyoelezwa katika Mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu katika sekta isiyo rasmi ya taka.

Kampuni zetu nne zimeshikana kuunga mkono taarifa hii na kanuni zinazoambatana, kudhihirisha kujitolea kwetu kwa suala hili na kuhimiza kwamba kanuni hizi zikubaliwe kwa upana zaidi na zitekelezwe kwa dharura. Tutafanya yafuatayo:

  • kuendeleza na kutumia kanuni hizi katika minyororo yetu ya thamani, kwa ushirikiano na mashirika ya wakusanyaji taka
  • kutoa ripoti ya hatua tulizopiga kila mwaka
  • kuwahimiza wengine wajiunge na Mpango wa Usawa katika Urejeshaji

Onyesha Nia

Tunabuni utaratibu wa kuomba kujiunga na mpango huu na tungependa kukufahamisha jinsi mchakato huo unavyoendelea.

Onyesha Nia